Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli ameunga mkono wazo la kuchukua maamuzi magumu lililopata umaarufu kupitia mchango wa mpinzani wake Edward Lowassa, alipokuwa bungeni miaka kadhaa iliyopita baada ya kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu kufuatia sakata la Richmond.

Akiongea kwa nyakati tofauti jana katika mikutano ya kampeni mkoani Mara, Dk Magufuli alibainisha kuwa nchi inashindwa kuendelea kimaendeleo kwa kuwa viongozi wameshindwa kuchukua maamuzi magumu.

“Hili la kuchukua maamuzi magumu na kwa wakati ndiyo limetufikisha hapa,” alisema Dk Mafuli.

Mgombea huyo alishangaa kuona kuwa nchi ina misitu mingi lakini watoto wanakaa chini darasani na kudai kuwa hatua hiyo inatokana na viongozi kutochukua maamuzi magumu.

“Hivi kuna sababu za watoto wetu kukaa chini wakati tuna misitu ya kutosha? Unakuta waziri wa maliasili yupo lakini ni maamuzi tu… mimi sitavumilia hayo, na waziri atakayekuwa legelege nitamwambia anipishe,” alisema Dk Magufuli.

Edward Lowassa ambaye hivi sasa amekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliwahi keueleza bungeni kuwa nchi inashindwa kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kuwa viongozi hawachukui maamuzi magumu bali wanaishia kulalamika tu.

“Hatuwezi kuwa na taifa la kulalamika, wananchi wanalalamika, viongozi wanalalamika.. lazima awepo mtu anaeweza kuchukua maamuzi magumu,” alisema Lowassa akiwa bungeni.

Hata hivyo, wazo la Lowassa kuhusu maamuzi ‘magumu’ lilipingwa wazi na baadhi ya wabunge wa CCM akiwemo Samuel Sitta ambaye hivi sasa ni mjumbe wa kamati ya kampeni wa chama hicho , aliyedai kuwa maamuzi magumu hufanywa hata na vichaa, na kwamba kinachotakiwa ni ‘maamuzi ya busara’.

 

 

Waangalizi Wa Uchaguzi Wa Kimataifa Watahadharishwa
Palestina Kupeperusha Bendera Ofisi Za UN, Israel Yapinga