Rais John Magufuli amesema kuwa bado kuna nafasi ya kufanya mazungumzo ya kutafuta maridhiano kuhusu uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliopangwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.

Rais ameyasema hayo jana jjijini Dar es Salaam kupitia hotuba yake kwa wajumbe wa Kidiplomasia kutoka mataifa mbalimbali, iliyosomwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya, iliyofanyika Ikulu.

Alisema kuwa bado kuna nafasi ya kufanya mazungumz0 ya kutafuta maridhiano kati ya pande mbili kuhusu namna ya kuendesha uchaguzi huo wa marudio kwa njia ya uwazi na haki lakini akasisitiza kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika kama ulivyopangwa.

Alisema kuwa ingawa Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, ina katiba yake na Tume yake ya Uchaguzi (ZEC) inayojitegemea na inayofanya maamuzi bila kuingiliwa.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuzungumzia uchaguzi wa marudio wa Zanzibar na kueleza msimamo wake wakati ambapo kumekuwa na mvutano kati ya vyama vikuu vyenye ushindani zaidi visiwani humo vya CCM na CUF.

CUF wameendelea kushikilia msimamo wao kuwa hawatashiriki uchaguzi huo wakidai ni batili na unaenda kinyume na katiba kwani uchaguzi ulishafanyika Oktoba 25 mwaka jana. CCM wameendelea kuwahimiza wanachama wao kushiriki kwa wingi katika zoezi la upigaji kura wa marudio.

Mvutano huu umeendelea baada ya juhudi za kutafuta maridhiano kupitia vikao mbalimbali vilivyowashirikisha marais wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na waliokuwa wagombea urais, Dk. Ali Mohammed Shein na Maalim Seif Sharif Hamad kushindwa kuzaa matunda chanya.

 

 

Kocha Mpya Wa Twiga Stars Ahimiza jambo Kikosini
Makamu wa Rais akanusha kuanzisha Vicoba, Saccos