Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imelikana zuio la kufanyika uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam lililotangazwa na Mkurugenzi wa Jiji hilo na kupelekea kuahirishwa kwa uchaguzi huo wikendi iliyopita na kuzua vurugu kubwa.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Waliarwande Lema alieleza kuwa ombi la zuio la uchaguzi huo lililowasilishwa mahakamani hapo na Saada Kimji na Suzan Massawe lilikufa baada ya mahakama kuweka zuio la muda lakini walalamikaji hawakuonekana mahakamani mara kadhaa kesi hiyo ilipopangwa kusikilizwa.

Alisema kuwa mahakama ilipanga tarehe ya mwisho ya kusikiliza shauri hilo ambayo ilikuwa Februari 23 mwaka huu lakini walalamikaji hawakutokea pia, hivyo ikalifutilia mbali.

Hakimu Lema alieleza dhahiri kuwa aliyesema kuwa Mahakama hiyo iliweka pingamizi dhidi ya uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa jiji la Dar es Salaam ni muongo huku akisisitiza kuwa zuio halali la mahaka hiyo lazima liwe na jina la Hakimu husika pamoja na sahihi yake.

Uchaguzi wa Meya wa jiji hilo ulipangwa kufanyika Februari 27 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, lakini uliahirishwa kutokana na madai ya kuwepo zuio la mahakama.

Madiwani na wabunge wa vyama vinavyounda Ukawa walifanya vurugu baada ya polisi kuwataka waondoke ukumbini muda mfupi baada ya Mkurugenzi wa jiji kutangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo. Tukio hilo limepelekea wabunge wa wa Kawe na Ubunge, Halima Mdee na Saed Kubenea pamoja na madiwani wengine wawili kushikiliwa na jeshi la polisi jana kwa mahojiano.

Jeshi la polisi pia limetangaza kumtafuta Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kwa ajili ya mahojiano kufutia tukio hilo.

January Makamba aikosoa Serikali ya JK
Video Mpya: Harmonize Feat. Diamond - Bado