Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa 12 kuchukue hatua stahiki kutatua tatizo la udumavu uliozidi wastani wa kitaifa, kwenye maeneo yao na kuhimiza lishe bora.
Majaliwa ametoa wito huo wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona.
Amesema, “taarifa zilizopo zinaonesha hali ya lishe miongoni mwa Watanzania hairidhishi kutokana na kuathiriwa na tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, uzito pungufu, ukondefu na uzito uliozidi pamoja na uliokithiri (kiribatumbo),” amesema.
Mikoa yenye kiwango kikubwa cha udumavu zaidi ya wastani wa kitaifa ni pamoja na Iringa inayoongoza kwa asilimia 56.9, Njombe (asilimia 50.4), Rukwa (asilimia 49.8), Geita (asilimia 38.6) na Ruvuma (asilimia 35.6).
Mingine ni Kagera (asilimia 34.3), Simiyu (asilimia 33.2), Tabora (asilimia 33.1), Katavi (asilimia 32.2), Manyara (asilimia 32), Songwe (asilimia 31.9) na Mbeya (asilimia 31.5), huku Viongozi wa Mikoa hiyo wakitakiwa kutafakari na kuchukua hatua stahiki.