Mama mzazi wa kiungo wa klabu ya Simba SC, Jonas Mkude, kwa mara ya kwanza amezungumzia sakata linalomuhusu mwanawe, ambaye alifikishwa mbele ya kamati ya nidhamu inayoongozwa na Mwenyekiti Seleman Kova, kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Mkude amekua akichukua sehemu kubwa ya habari za michezo katika siku za karibuni, hasa baada ya kamati ya nidhamu ya Simba SC, kuagiza mchezaji huyo apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili ili akapimwe akili.

Mama mzazi wa kiungo huyo aliedumu kwa muda mrefu Simba SC aitwaye Grace, amesema sakata hilo linamuumiza, hasa baada ya kusikia Jonas ametakiwa kupimwa akili.

“Imeniumiza sana kwani nimemzaa Jonas akiwa na akili timamu na nimeyaona yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii yananipa mawazo ila sina chakufanya.

“Utumbo unanikata kwani nimembeba miezi tisa tumboni kwangu, ilinishtua sana kuambiwa anatakiwa kwenda kupima wengine wakidai akili, ila namuombea kwa Mungu amlinde.”

“Nilimzaa akiwa mzima, pia anapaswa kumuomba Mungu amsimamie, ujue siwezi kuingilia mambo ya ajira yake ila imenigusa kuhusu akili yake,”

“Asubiri maamuzi na klabu, ndio maana nimesema hilo siwezi kuliingilia, pia anapaswa kunyamaza kimya na sio kujibizana na kila mtu,”

Hata hivyo mpaka sasa haijulikani ni lini kamati ya nidhamu ya Simba SC itakutana kujadili suala la kiungo huyo, huku ikisemekama amegoma kupimwa, kama alivyotakiwa ili kujiridhisha hana tatizo lolote kiakili.

Mkude alinza kucheza kikosi cha kwanza cha Simba SC msimu wa 2011, akitokea kikosi cha vijana, na kwa sasa ni mmoja wa wachezaji walioitumikia timu hiyo kwa muda mrefu.

Dkt. Gwajima: Makatibu wa Afya hili ni jukumu lenu
Sabaya afikishwa Mahakamani wananchi wamzomea