Mashetani wekundu Man Utd, wameshindwa kufurukuta mbele ya mabingwa wa soka nchini Ufaransa PSG, baada ya kutandikwa bakora mbili kwa sifuri katika mchezo wa kujiandaa na msimu mpya wa ligi.

Man Utd ambao wamekua na mazingira mazuri ya kupata ushindi katika michezo yao ya kirafiki iliyopita, iliyochezwa huko nchini Marekani walijikuta wakilamba kisago hicho kufuatia uwezo mzuri ulioonyeshwa na wapinzani wao kutoka Ufaransa.

Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic aliifungia PSG bao la pili katika dakika ya 34, baada ya kiungo kutoka nchini Ufaransa, Blaise Matuidi kufunga bao la kwanza katika dakika ya 25.

Katika mchezo huo mlinda mlango wa Man Utd, David De Gea alionekana kucheza chini ya kiwango na kocha wa Man Utd, Louis van Gaal alimtoa baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Kutokana na hali hiyo, Van Gaal sasa anawaza mawili, amruhusu aende Real Madrid au ampe mkataba mwingine, lakini kizungumti kingine kinachomkabili meneja huyo kutoka nchini Uholanzi ni kuamini De Gea ana mtazamo chanya (uzoefu) katika kikosi chake kwa sasa.

David De Gea amekuwa akihusishwa sana kuhamia Real Madrid, ingawa uongozi wa Man Utd umekua ukiweka msimamo wa kutomrusu kuondoka.

Mchezo huo wa kirafiki dhidi ya PSG umekua wa mwisho kwa mabingwa hao wa kihistoria katika soka la nchini England, na sasa watarejea nyumbani kumalizia sehemu ya maandalizi kabla ya kuanza kwa ligi mwishoni mwa juma lijalo.

Manchester United wataanza kurusha karata yao ya kwanza katika ligi ya nchini England dhidi ya Tottenham mnamo Agosti 8 mwaka huu.

Walichokisema Makocha Baada Ya Yanga Kupigwa Na Azam FC
Mwigulu Nchemba Apangua Gia Tuhuma Za Rushwa