Jeshi la Polisi nchini, kupitia Polisi jamii kwa kushirikiana na Wananchi na Watendaji kata, limekuja na mpango kazi wa kuzuia matukio ya mauaji Mkoani Kagera, mengi yakihusishwa na migogoro ya ardhi, mapenzi na ushirikina.
Hatua hiyo, imewasilishwa katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Polisi mjini Bukoba na kilichowahusisha Viongozi wa dini, watendaji wa kata na kamati ya ulinzi ya mkoa.
Kamishna wa Polisi jamii, Jeshi la Polisi nchini, Faustine Shilogile akiongea katika kikao hicho, amewaelekeza watendaji wa kata na viongozi wa mitaa, kufuatilia na kuwabaini watu wanajihusisha na matukio hayo.
Amesema, “turudi katika maeneo yetu na tuhakikishe kwamba maeneo yetu hayo yanakuwa salama kwa kutoa elimu na kujihakikishia kwamba tunafatilia watu wanaojihusisha na haya mauaji.”
Aidha, ameongeza kuwa, Mkoa wa Kagera mpaka sasa yametokea matukio 35 ya mauaji kwa mwezi January pekee huku asilimia kubwa yakihusishwa na wivu wa kimapenzi, migogoro ya ardhi na ushirikina.