Mkuu wa Habari na Mawasiliano ya klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kikosi chao kitakua cha kwanza kupeleka kilio Jangwani msimu huu 2021/22.

Ruvu Shooting watashuka dimbani (Uwanja wa Mkapa) leo Jumanne ‘Novemba 02’ saa kumi na mbili jioni, kuikabili Young Africans.

Masau Bwire amesema kikosi chao kimejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo huo, na wana matumaini ya kuibuka na ushindi, ambao utakua kilio cha kwanza kwa wapinzani wao msimu huu.

Amesema Wadau wengi wa soka wanaipa uhakika mkubwa wa Young Africans kushinda mchezo huo, lakini mambo yatakuwa tofauti kwa sababu Ruvu Shooting imejiandaa vizuri kuchukua alama 3 leo, na kuhakikisha itatwaa ubingwa wa Ligi msimu huu.

“Tumejipanga kushinda mchezo wa leo dhidi ya Young Africans, tuna imani hiyo japo wadau wengi wa soka wanatubeza,” amesema Masau Bwire.

Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 12, zilizotokana na ushindi walioupata kwenye michezo minne waliocheza, huku Ruvu Shooting wakiwa nafasi ya nane kwa kumiliki alama 04.

Mrithi wa Gomes kutangazwa juma hili
Shahidi wa Tano akitoa ushahidi kesi ya kina Mbowe