Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amekemea vikali vitendo vya mauaji vinavyojitokeza mkoani Tabora na kuwataka wakazi wa mkoa huo kuacha kujichukulia sheria mikononi.
Dkt. Mpango ametoa maagizo hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora inayogharimu shilingi Bilioni 2.8 iliopo katika kata ya Mpela mtaa wa Uledi Manispaa ya Tabora.
Amesema, wakazi hao wanatakiwa kutumia njia ya mazungumzo kwa kushirikisha wazee pamoja na viongozi wa dini pamoja na kufuata mkondo wa sheria pale panapotokea migogoro katika familia au jamii.
Kuhusu Ujenzi wa Hospitali hiyo, Dkt. Mpango ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Tabora kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU kuhakikisha wanamfikisha katika vyombo vya sheria aliyefanya ubadhirifu wakati wa Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora.