Mbunge wa Jimbo la Ukerewe mkoani Mwanza kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Michael Mkundi ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya ubunge na nyazifa zote ndani ya chama hicho.

Amesema kuwa ameamua kuchukua uamuzi huo mara baada ya kusema chama hicho kimepoteza heshima na utu, baada ya kumtelekeza katika kipindi ambacho alihitaji msaada na mshikamano kutoka kwenye uongozi wa chama chake kipindi cha ajali ya kivuko cha MV. Nyerere.

Aidha, mbunge huyo ameomba kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili aweze kufanya siasa za maendeleo na kuwasaidia wananchi.

“Kwa msingi huu nimeamua kujivua uanachama wa Chadema, na hii ikiwa ni kwa mujibu wa Katiba ya Chadema Ibara ya 5.4.1 chama ambacho kwa tiketi yake nimekuwa diwani wa Kata ya Bukiko na mbunge wa jimbo la Ukerewe, kwa kujivua uanachama natangaza pia kujiuzulu nafasi ya udiwani na ubunge wa jimbo la Ukerewe,”amesema Mkundi

Hata hivyo, ameongeza kuwa katika kipindi hiki akiwa mtu huru, amesema amejipanga kushiriki kikamilifu katika tume iliyoundwa na waziri mkuu Kassim Majaliwa kuchunguza ajali ya MV. Nyerere na masuala mazima ya usafiri majini.

Mambosasa: Tukio hili limefanywa na wazungu wawili
Al-Shabab watangaza kuwaua wapelelezi wa Marekani, Uingereza