Kocha Mkuu wa Kikosi cha Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema licha ya timu ya taifa, Taifa Stars kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Uganda lakini wachezaji wanapaswa kupongezwa kwa kazi waliyoifanya.

Maxime ameeleza hayo kufuatia baadhi ya wadau wa Soka la Bongo kupishana kauli baada ya kichapo hicho, huku akisisitiza kuwa mbali na matokeo hayo lakini vijana walijitahidi kupambana na kwamba haikuwa riziki yao na ushindi ukatua kwa Uganda.

Amesema kuwa wanapaswa kupongezwa na si kukatishwa tamaa kwani bado kuna nafasi ya mechi mbili za kufanya vizuri kufuzu Fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazofanyika Ivory Coast mapema mwaka 2024.

“Inabidi tuwapongeze wamepambana kwa kiasi chao lakini yote kwa yote haikuwa riziki yetu, wao (Uganda) wamepata ushindi lakini kikubwa ni kuwapongeza wachezaji maana bado wana nafasi, tuna mechi mbili tusikate tamaa,” amesema Maxime ambaye aliwahi kuwa nahodha wa Taifa Stars.

Amesema kiufundi timu hiyo ilipoteza mchezo huo uliopigwa Jumanne, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam baada ya kutoka kwa viungo, Mzamiru Yassin na Himid Mao ambao kwa kiasi kikubwa waliidhibiti Uganda eneo la katikati ambalo walikuwa hatari zaidi.

Katika Msimamo wa wa Kundi F, Taifa Stars inashikilia nafasi ya pili kwa kuwa na alama 04 sawa na Uganda inayoshika nafasi ya tatu, huku Algeria ikishafuzu kwa kufikisha alama 12 na Niger inaburuza mkia kwa kuwa na alama 02.

Mradi ufugaji Jongoo Bahari kuwaneemesha Wananchi
Rais Samia azindua Kamati tathmini utendaji Wizara Mambo ya nje