Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo ameshuhudia uwekaji saini wa mkataba baina ya EU na
Shirika la Maendeleo la Ufaransa – AFD, ambapo EU imetoa msaada kwa Tanzania wa Euro milioni 36 sawa na Shilingi bilioni 95 kwa ajili ya Mradi
wa Uzalishaji wa Umeme kwa njia ya Maji wa Kakono, mkoani Kagera wa MW 87.8.

Uwekaji saini huo, ulifanyika wakati wa Mkutano wa Global Gateway Forum uliofanyika Brussels, Ubelgiji Oktoba 25-26, 2023 ambapo Prof.
Mkumbo alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo.

Mradi huo wenye gharama ya jumla ya Euro million 288.11 sawa na takribani Shilingi bilioni 800 unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kupitia mikopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa -AFP, Benki ya Maendeleo
ya Afrika – AfDB na msaada wa EU.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (kushoto) akifurahia baada ya uwekaji saini wa mkataba baina ya EU na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ambapo EU imetoa msaada kwa Tanzania wa Euro milioni 36 sawa na Shilingi bilioni 95 kwa ajili ya Mradi wa Uzalishaji wa Umeme kwa njia ya Maji wa Kakono, Mkoani Kagera wa MW 87.8).

Taarifa ya Ubalozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji imesema, Mkumbo ameishukuru EU kwa msaada wake kwenye Mradi huo na kuahidi kuwa Serikali itasimamia kikamilifu utekelezaji wake ambapo pia alishiriki na kuchangia kwenye mijadala yenye lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya masuala madini kimkakati na mageuzi ya kidijitali.

Kuhusu madini ya kimkakati, majadiliano na
makubaliano yamefikiwa kwamba Mpango wa Global Gateway uchochee uwekezaji unaowezesha madini ya kimkakati kuongezewa thamani katika nchi yanakochimbwa badala ya thamani kuongezwa baada ya madini hayo
kuuzwa nje.

Tanzania ni nchi yenye karibu aina zote za madini hayo ikiwemo lithium, graphite, cobalt na nickel, Mhe. Waziri ameuhakikishia Mkutano huo utayari
wa Serikali kupokea uwekezaji huo na tayari mazingira mazuri na rafiki ya uwekezaji yamewekwa huku upande wa mageuzi ya kidijitali, Waziri ametumia Jukwaa hilo kuishukuru EU kwa msaada wa Euro milioni 35 sawa na shilingi bilioni 80 ilizotenga kuisaidia Tanzania kwa ajili ya kuchochea mageuzi ya kidijitali.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila A. Mkumbo (wa pili kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas A. Nyamanga (wa kwanza kulia) wakifutilia majadiliano ya Mkutano wa Global Gateway Forum uliofanyika Brussels, Ubelgiji Oktoba 25-26, 2023.

Wajumbe waliafikiana kuwa mageuzi ya kidijitali yatumike kuongeza kasi ya uwekezaji katika maeneo yanayochochea maendeleo ya kidijitali kama vile Kilimo, Elimu, Biashara, Afya na mengineyo na kuhimiza mageuzi ya kidijitali yachochee zaidi maendeleo ya wananchi wakiwemo wa vijijini.

Aidha Waziri Mkumbo alitumia fursa hiyo pia kufanya mikutano ya pembezoni na uongozi wa juu wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya – EIB, kueleza mipango na vipaumbele mbalimbali vya kitaifa na kuomba Benki hiyo iendelee kushirikiana na Serikali yetu katika utekelezaji wa mipango na vipaumbele hivyo kupitia mikopo ya masharti nafuu.

EIB ni mmoja wa wabia wa maendeleo na kupitia mikopo nafuu ya Benki hiyo miradi mbalimbali hivi sasa inatekelezwa ikiwamo ya ukarabati wa
baadhi ya viwanja vya ndege, miradi ya maji na mikopo kwa ajili ya wajasiriamali kupitia benki za Tanzania.

Vile vile, Prof. Mkumbo alizungumza na Mkurugenzi anayeshughulikia Ubia wa kimataifa
ndani ya EU kwa nchi za Afrika na kujadiliana mipango na vipaumbele vya Tanzania ambapo wakati wa majadiliano hayo, aliishukuru EU kwa
msaada wa Euro milioni 703 ambazo ni takribani shilingi trilioni 1.9 ilizopanga kusaidia kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2027.

Global Gateway Investment Package ni mpango wa EU wa kuchochea uwekezaji duniani hususan barani Afrika ambako Mpango huo unalenga
kuchochea uwekezaji wa jumla ya Euro billioni 150 barani Afrika ambapo Nchi zaidi ya 90 zilihudhuria mkutano huo kwa ngazi ya Marais, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri pamoja na viongozi wengine kutoka Mashirika ya Kimataifa na sekta binafsi.

Watendaji, Wenyeviti epukeni migogoro ya Ardhi - DC Malisa
Miundombinu Mahakama ya udhalilishaji iboreshwe - TAMWA ZNZ