Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa kesho anatarajiwa kutangaza kikosi chake kwa ajili ya mechi mbili za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Chad.

Mkwasa anatarajiwa kutangaza kikosi ambacho hakitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa sana kutokana na viwango vya wachezaji waliopo Taifa Stars na wale ambao wanaopigania kuitwa.

Swali kubwa ni pengo la Nadir Haroub ambaye alikuwa akiunda safu ya ulinzi pamoja na pacha wake wa klabuni, Kelvin Yondani.

Beki huyo mkongwe ambaye ameitumikia Taifa Stars kwa miaka kadhaa alitangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa kufuatia kuvuliwa unahodha na jukumu hilo kukabidhiwa kwa Mbwana Samatta.

Aggrey Morris alitarajiwa kuwa mbadala wa Cannavaro lakini amekuwa nje kwa muda mrefu kwenye klabu yake ya Azam kutokana kuwa na majeruhi hivyo kushindwa kuthibitisha makali yake mbele ya macho ya Mkwasa ambaye huenda angemzingatia kwa kumjumuisha kikosini.

David Mwantika wa Azam ambaye amekuwa akicheza na Pascal wawa anaweza kutupiwa jicho na Mkwasa kama ilivyo kwa Erasto Nyoni ambaye anamudu kucheza katikati na pembeni.

Balozi Sefue: Najisikia nimeheshimika sana
Azam FC Kuifuata Bidvest Sauzi J5