Kiungo kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Newcastle Utd Moussa Sissoko, bado ana matarajio ya kutimkia mjini Madrid na kujiunga na mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.

Sissoko amekua na wazo la kuondoka Newcastle Utd, tangu alipokua katika fainali za mataifa ya barani Ulaya (Euro 2016), ambapo alionekana kuwa na kiwango cha hali ya juu akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa ambayo ilishindwa kubakisha ubingwa wa michuano hiyo nyumbani.

“Nina matumaini Real watanisajili, bado ninasubiri,”

“Kama Real Madrid wamevutiwa na uwezo wangu na tayari nimeshasikia taarifa hizi, sina shaka na mpango huo, naamini nitaondoka kabla ya dirisha kufungwa mwishoni mwa mwezi huu.” Alisema Sissoko alipohojiwa na shirika la utangazaji la Uingereza (BBC).

Pamoja na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 kuwa na matarajio hayo, bado uongozi wa klabu ya Newcastle Utd haujapokea ofa yoyote kutoka Real Madrid ama klabu nyingine ambayo imethubutu kuonyesha nia ya kumsajili.

Tayari meneja wa Newcastle Utd Rafael Benitez ameshakata tamaa juu ya kumtumia Sissoko katika kikosi chake ambacho tayari kimeshaanza mshike mshike wa ligi daraja la kwanza tangu mwishoni mwa juma lililopita, ameshatoa ruhusa ya kuondoka kwake kama ofa itatua ofisini kwake.

Pascal Wawa Aanza Rasmi Mazoezi, Aahidi Makubwa 2016/17
Man Utd, Chelsea Zakabana Koo Kwa Wabrazil