Ikiwa ni siku moja baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kumpa onyo kali mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kwa kauli zake dhidi ya mhimili huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa naye ameuchokoza moto huo.

Msigwa ambaye yuko jijini Nairobi katika hospitali ya Aga Khan alipolazwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ameandika ujumbe Twitter na Instagram unaokosoa vikali kauli ya Spika Ndugai kuhusu Mbunge wa CCM kukodi ndege iliyombeba Lissu baada ya kushambuliwa kwa risasi.

Spika Ndugai ameripotiwa kuliambia Bunge kuwa Mbunge wa CCM ndiye aliyeagiza ndege kutoka Nairobi kwa dola za Kimarekani 9,200 kumsafirisha Lissu na kwamba angerejeshewa kiasi hicho.

Msingwa ameandika kupitia Twitter, “Spika Ndugai muogope Mungu, usilete utani na katika maisha ya Mh Lissu, umeliongopea Bunge na umma, gharama zote za ndege zimelipwa na CHADEMA na Watanzania. The Parliament deserves better that you!”

Jana, Spika Ndugai aliwaonya wabunge dhidi ya kauli zinazolenga kudhalilisha au kushambulia muhimili huo kwenye mitandao ya kijamii kwani kuna Kamati za Bunge ambazo wangeweza kwenda kufikisha maoni na malalamiko yao. Alimshukia pia Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea kwa kauli yake aliyoitoa katika Kanisa la Ufufuo na uzima akidai Spika hakueleza ukweli kuhusu idadi ya risasi zilizotumika kumshambulia Lissu.

Leo, Spika ametangaza kumsamehe mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwa kauli zake dhidi ya muhimili huo akieleza kuwa ‘hajui alitendalo kwa maneno aliyoyasema barabarani’.

Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari lake, nyumbani kwake eneo la Area D mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kutoka Bungeni.

Video: Itazame ngoma mpya ya Rayvanny 'Unaibiwa'
Taifa Stars yashuka viwango vya FIFA