Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema inatambua umuhimu wa mapitio ya mitaala ambayo yataongeza masomo na kozi mbalimbali zilizojikita kutoa zaidi ujuzi utakao wawezesha wahitimu kujiajiri.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma na kusema pia wamepokea ushauri wa Mbunge wa Viti Maalum, Naghenjwa Kaboyoka ya kutumia bidhaa zitokanazo na ubunifu wa wanafunzi kuingizia kipato shuleni.
Katika Swali lake la msingi, Mbunge huyo aliitaka kufahamu endapo serikali inaona umuhimu wa kuanzisha masomo yatakayoibua vipaji vya watoto ambapo Naibu Waziri alisema Serikali inatambua umuhimu wa masomo yanayoibua vipaji vya watoto kuanzia ngazi ya Elimu ya Msingi.
Aidha, amesema katika masomo hayo mada mbalimbali zinazochochea vipaji zinafundishwana kwamba upande wa somo la Sayansi na Teknolojia, wanafunzi hujifunza Matumizi ya Nishati, Majaribio ya Kisayansi, Mashine na Kazi na Kuelea na Kuzama kwa vitu.