Serikali nchini, imesema imepanga kuijumuisha lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini kwa lengo la kutatua changamoto ya mawasiliano zinazowakabili wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Deogratius Ndejembi ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa mchakato wa mapitio ya sera na mitaala unaoendelea unapendekezwa ulazima wa somo hilo.
Amesema, “Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa mpango na mapendekezo hayo, serikali imeandaa na kusambaza kamusi ya lugha ya alama ya Tanzania ya kidijitali katika shule na vyuo vinavyopokea wanafunzi viziwi.”
Kauli ya Ndejembi inakuja kufuatia swali la Mbunge wa Viti Maalum, Stella Ikupa kutaka kujua mpango wa Serikali kuingiza lugha ya alama kwenye Mitaala ya Elimu ambapo pia Ndejembi amesema mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari yatawajengea uwezo wa kuwafundisha na kuwahudumia wanafunzi viziwi.