Uongozi wa klabu ya Mtibwa Sugar umeshikwa na kigugumizi kuhusu suala la kuondoka kwa kocha Hitimana Thiery, ambaye usiku wa kuamkia jana Jumatano (April 07), aliweka hadharani taarifa za kuachana na klabu hiyo.

Kocha Hitimana alikabidhiwa kikosi cha Mtibwa Sugar Disemba 2020, baada ya kuondoka kwa aliyekua kocha klabuni hapo Zubery Katwila aliyejiunga na Ihefu FC.

Afisa habari wa Mtibwa Sugar, Tobias Kifaru amezungumza na Dar24 Media, ambapo amesema taarifa za kuondoka kwa kocha huyo sio za kweli na uongozi wa juu klabuni hapo unafanya mchakato wa kumtumia tiketi ili aweze kurejea jijini Dar es salaam, akitokea kwao Rwanda.

Kifaru amesema taarifa za kuondoka kwa kocha huyo zimezushwa na wakati wowote zitatolewa ufafanuzi wa kina na uongozi wa klabu hiyo yenye maskani makuu wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

“Kocha Hitimana bado ni sehemu ya benchi la ufundi la timu yetu, hata mimi nimeshtushwa na taarifa hizi lakini nikuhakikishie kuwa Hitimana atarejea nchini na huenda akawepo kwenye mchezo wetu dhidi ya Azam FC utakaochezwa kesho Ijumaa, jijini Dar es salaam.”

“Uongozi wetu utalitolea ufafanuzi wa kina suala hili, kwa sasa unaangalia sana mchezo wetu dhidi ya Azam FC ambao tumedhamiria kuwafunga kama tulivyofanya kwenye mzunguuko wa kwanza, tulipocheza kwenye Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro.” Amesema Kifaru

Hitimana Thiery kwa sasa yupo nchini kwao Rwanda alipokwenda kwa ajili ya mapumziko, na hakushiriki kwenye maandalizi ya kikosi cha Mtibwa Sugar kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC.

Mo Dewji: Bilionea pekee kutoka Afrika Mashariki katika orodha ya Mabilionea 18 Afrika
Rais wa Afrika Kusini amteua Mo Dewji kuishauri serikali ya nchi hiyo