Kila Jiji duniani lina wababe wake na ubabe wa maana ni ule ubabe wa kusimamia taratibu, na enzi hizo, David Mwaibula alikuwa ni mmoja wa wababe wa Dar es Salaam kwenye kusimamia taratibu.

Hakika, alikuwa ni msimamizi mkuu na mahiri wa masuala ya Daladala jijini na huyu alikuwa haswa ‘ Mzee wa Daladala’ maana mbali ya mabadiliko mengine, ndiye aliyeasisi utaratibu wa madereva na makondakta wa Daladala kuvaa sare.

Na jamaa alikuwa mbabe haswa akimkuta kondakta amevaa kandambili alimshusha na kumwambia arudi nyumbani akafuate viatu vyake, maana kwa Mwaibula, mtu ni lazima alikuwa aheshimu kazi yake, huwezi kwenda kazini na kandambili.

David Mwaibula.

Mwaibula alibuni ruti mpya nyingi za Daladala, ndiye aliyeanzisha pia utaratibu wa Daladala kuwa na mikanda ya rangi kuonyesha ni ya route gani, aidha, kuandika mbele kwa rangi na maandishi makubwa kama ni Temeke – Posta au Kariakoo kwani makonda walikuwa na tabia ya kubadilisha vibao vya ruti zao.

Mara kadhaa Mwaibula alijichukulia sheria mkononi na hata kuwatandika viboko madereva na makondakta waliokatisha ruti, kwa wale makonda ambao hawakuwa nadhifu kazini basi kila walipomuona mwamba huyu walitoka mbio kwenda kuvalia vizuri sare zao za kazi

Mwaibula ndiye pekee mjini aliyekuwa akiendesha Benzi iliyotumika Ikulu ya Nyerere.
Aliwezaje kununua Benzi chakavu ya Ikulu?
Ni Tafakuri Jadidi.

Daladala jijini Dar es Salaam.

Lakini Benz hilo lilikuwa maarufu na kila dereva na konda wa Daladala alilijua vizuri kwani kila lilipoonekana sehemu basi taratibu zilizingatiwa kwa heshima na taadhima.

Daladala.

Huyu alisaidia sana kuweka utaratibu wa makonda kutoning’inia mlangoni gari likiwa barabarani na utaratibu wa kufunga mlango Daladala linapotoka stendi na kiufupi aliheshimika na kuogopwa na makonda kuliko hata wanavyowaheshimu Askari wa Usalama Barabarani.

Huyu alikuwa mteule wa Rais Mkapa kwenye tume ya Jiji baada ya kuvunjwa Halmashauri zote za Jiji, na ndipo alipokabidhiwa kitengo cha Daladala na kuweka umwamba wake uliodumu hadi leo.

Waziri Ummy: Hakuna maambukizi mapya Kagera
Mama Janeth Magufuli atunukiwa Tuzo ya Heshima