Mahakama ya kijeshi nchini Cameroon imemhukumu kifungo cha maisha jela, kiongozi wa vuguvugu la eneo linalozungumza kingereza, Julius Sisiku Ayuk Tabe, hukumu ambayo wadadisi wa mambo wanasema huenda ikachochea machafuko zaidi.
Tabe anayeonekana kama kiongozi mwenye msimamo wa kati katika vuguvugu linalodai eneo hilo kujitenga, amehukumiwa sambamba na watu wengine 9 kwa makosa ya ugaidi na kuendesha harakati hatari kwa usalama wa taifa.
Aidha, hukumu hiyo imethibitishwa na wakili wa vuguvugu hilo, Joseph Fru, ambaye amesema kuwa watu wengine 10 walitakiwa kulipa faini ya CFA bilioni 250, sawa na dola za Marekani milioni 422.
Hata hivyo, Fru amelaani na kusema kuwa hukumu hiyo ni yakushangaza na kwamba wateja wake wote wamekataa kutambua mamlaka ya mahakama ya kijeshi iliyokuwa inasikiliza kesi hiyo jijini Yaounde.
Tabe mwenye umri wa miaka 54 na mtaalamu wa masuala ya TEHAMA, alijitangaza kama rais wa Ambazonia, jimbo lililojitenga na Cameroon mwezi October 2017, ambapo Serikali iliingilia kati kwa kutuma wanajeshi ambapo watu 1800 waliuawa.