Ndege iliyobeba mwili wa aliyekuwa Rais wa Angola, José Eduardo dos Santos ambaye alifariki nchini Hispania Julai 8, 2022 imewasili jijini Luanda, Angola baada ya vita vya kisheria vya kugombania mwili huo vilivyodumu kwa mwezi mmoja.

Mwili huo, mara baada ya kuwasili ulipelekwa katika makazi ya kiongozi huyo wa zamani katika eneo la Miramar ambapo mjane wake, watoto watatu na jamaa wa karibu walipokea rambirambi kutoka kwa watu waliotembelea nyumba yao.

Magari ya msafara, kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro hadi Miramar, yalikuwa yamezungukwa na watu waliojipanga barabarani kutoa heshima zao kwa Rais huyo aliyeongoza Angola kwa miaka 38.

Aliyekuwa Rais wa Angola, Hayati José Eduardo dos Santos. Picha na Club for Mozambique.

Marcy Lopes, ambaye yuko katika tume inayoandaa hafla ya mazishi ya Dos Santos, alisema kwamba “tarehe na programu ya mazishi itatangazwa hapo baadaye mara baada ya taratibu kukamilika.”

Awali, msemaji wa chama tawala cha People’s Movement for the Liberation of Angola (MPLA), alisema “mazishi yangefanyika jijini Luanda Agosti 28, tarehe ambayo Dos Santos angetimiza miaka 80.”

Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari nchini Angola vimesema Serikali inayoongozwa na Rais João Lourenço inakusudia kufanya mazishi siku ya Jumatatu Agosti 22, siku mbili kabla ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kufanya uchaguzi wake mkuu.

Msafara uliopokea mwili wa Dos Santos ukielekea kwenye makazi yake eneo la Miramar jijini Luanda. Picha na Arnaldo Vieira.

Wakati huo huo, pande mbili za familia ya rais huyo wa zamani ziko katika mzozo wa Familia katika Mahakama ya Kiraia ya Catalonia kuhusu ni nani anayepaswa kuulinda mwili wa Dos Santos.

Upande wa pili ni mjane Ana Paula dos Santos na wanawe ambao pia wanadai mwili huo na kutaka uzikwe nchini Angola siku za usoni.

Kenya: Odinga awaambia Viongozi wa Dini ana ushahidi wa kutosha
Augustino Lyatonga Mrema afariki