Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amewataka wachezaji wake kusahau matokeo yaliyopita na kuelekeza akili na mawazo yao kwenye mchezo wa kesho Jumapili (April 02) dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

Katika mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika, uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam miamba hiyo ya Tanzania iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kocha Nabi amesema pamoja na wenyeji wao TP Mazembe kutokuwa na nafasi ya kusonga mbele, lakini wanahitaji kupata ushindi ili kumaliza kwa heshima michezo ya hatua ya makundi.

“Tunapaswa kuthibitisha ubora wetu kwa kushinda ugenini mbele ya TP Mazembe, ili hilo lifanikiwe lazima kusahau matokeo yaliyopita na kutowadharau wapinzani kwa mwenendo mbovu waliokuwa nao, lazima kila mmoja wetu awajibike ili tufikie malengo kwenye mchezo huu,” amesema Nabi.

Kocha huyo kutoka nchini Tunisia ameeleza kuwa mapokezi mazuri waliyoyapata Lubumbashi kutoka kwa wenyeji wao pamoja na kundi kubwa la mashabiki kuonekana kuwaunga mkono havitoshi kuwapa alama tatu, bali kitu cha msingi ni kucheza kwa kupambana muda wote wa mchezo.

Kwa upande wake meneja wa timu hiyo, Walter Harson ameeleza kuwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi yanakwenda vizuri na wachezaji wote wakiwemo wale waliokuwa kwenye timu zao za taifa wameshaungana na wenzao kambini Lubumbashi.

Doumbia afunguka kinachomkwamisha Young Africans
Ahmed Ally: Simba SC imeweka Rekodi Morocco