Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo ameeleza kusikitishwa na hali ya uchumi wa wananchi nchini huku akitaka wananchi wasimlaumu Rais John Magufuli kwa hali hiyo.

Mwanasiasa huyo mkongwe amesema kuwa hivi sasa wananchi wamekuwa katika wakati mgumu kifedha kutokana na kukosekana kwa mzunguko wa fedha na kwamba wanaopaswa kulaumiwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama taasisi ambayo ilimdhamini Rais Magufuli kuinadi na kutekeleza ilani yake.

“Rais Magufuli amedhaminiwa na CCM, hivyo bila CCM Magufuli asingekalia kiti hicho. CCM ndiyo inapaswa kumsimamia mtu wao aongoze nchi ili kila mmoja afurahie utawala wake,” Ndesamburo anakaririwa na Mwananchi.

“Leo kila mtu anamlaumu Rais Magufuli, tunafanya makosa. Tunapaswa kuilaumu CCM iliyowaaminisha wananchi kuwa Magufuli ni kiongozi bora,” aliongeza.

Aidha, Ndesambulo alizungumzia auamuzi wa Rais Magufuli kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020 ambapo alidai anachokifanya ni kujijenga yeye kwa ajili ya uchaguzi huo lakini CCM kama taasisi haijengeki. Alisema kwa mwenendo huo huenda CCM ikapoteza wabunge wengi mwaka 2020.

“Mwanzoni watu walifikiri ni upinzani tu wangeisoma namba, lakini sasa hivi hata CCM wenyewe wanaisoma namba. Masikini na matajiri wanaisoma namba kwa sababu ya uamuzi wa CCM,” Ndesambulo alisema.

Hata hivyo, hoja za Ndesamburo zilipingwa vikali na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka ambaye alidai kuwa wanaopaswa kulaumiwa ni viongozi wa vyama vya upinzani.

“Rais Magufuli yuko mstari sahihi kabisa bali wa kulaumiwa ni wapinzani waliotaka kuvuruga amani yetu ili kuwafurahisha waliowatuma kwa nia ya kutetea ufisadi,” alisema Ole Sendeka.

“Katika kampeni zao walikuwa wanasema wanataka kiongozi mwenye uamuzi, sasa amekuja Rais Magufuli anafanya uamuzi tatizo liko wapi? Alihoji.

Alisema kuwa Serikali ya CCM haitapoteza muda hata kidogo kukaa na viongozi wa upinzani kujadili kuhusu mipango yao ya kutaka kuvuruga amani ya nchi na badala yake wataendelea kujitika katika kuwaletea wananchi maendeleo hadi mwaka 2020 watakapopimwa tena na wananchi.

Ibada ya Hijjah Yafikia Kilele Chake Mlima Arafat
Vita Kuu Yanukia Kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini