Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), imesema maafisa maendeleo ya jamii ndilo daraja muhimu kwa makundi maalum ambayo ni wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kupata fursa za zabuni za umma zilizotengwa kwa ajili yao.
Hayo, yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Eliakim Maswi wakati alipokuwa akizungumza na Wakuu wa Vitengo na Idara za Maendeleo ya Jamii walipokutana kwenye kikao kazi hivi karibuni, jijini Dodoma.
Maswi aliwaambia maafisa hao kuwa, baada PPRA kufanya kampeni maalum ya kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum kwenye zabuni za umma kwenye mikoa saba nchini, imebaini kuwa hatua ya usajili wa makundi maalum ambayo ni jukumu la maafisa maendeleo ya jamii ni muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali.
Kupitia kampeni hiyo, iliyofanyika mikoa ya Rukwa, Tabora, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mtwara na Manyara, PPRA ilibaini kuwa maafisa maendeleo ya jamii wengi hawakuwa na uelewa kuhusu uwepo wa fursa hizi hali iliyosababisha kuwa na vikwazo na urasimu katika baadhi ya Halmashauri, hatua ambayo inafifisha juhudi za Serikali katika kuwawezesha wananchi kupitia makundi maalum.
Maswi amesema, “Uzoefu tuliopata kupitia kampeni ya elimu kwa umma kuhusu hizi fursa za makundi maalum, ambapo mwaka huu wa fedha kuna zaidi ya Shilingi trilioni tisa (9,000,000,000/=) zilizotengwa kwa ajili ya haya makundi maalum, tumebaini kulikuwa na vikwazo na urasimu ambao unakwamisha usajili,” alisema Bw. Maswi na kuwataka maafisa hao kuboresha utendaji wao wa kazi katika eneo hilo.”
Aidha, ameongeza kuwa anatarajia kuwa endapo wataboresha utendaji wao katika usajili wa vikundi, kutakuwa na ongezeko la vikundi nchini vitakavyoorodheshwa na PPRA kwa ajili ya fursa hizo, kwani hadi sasa kuna vikundi 195 pekee kwa nchi nzima vilivyoorodheshwa, idadi ambayo haiendani na uhitaji na ukubwa wa nchi.
Aliwataka maafisa hao kuiga mfano wa wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na viongozi wengine katika mikoa waliyotembelea ambao walionesha ushirikiano mzuri katika kufanikisha kampeni hiyo ambayo itaongeza fursa za ajira na kusaidia kuboresha maisha ya wananchi kupitia ununuzi wa umma.
“Kwa pamoja, kwa kushirikiana na Wizara inayohusika na vikundi maalum, tunaweza kupata suluhu na kuweka mazingira rafiki zaidi ya kusajili vikundi. Natoa wito kwenu, kila mmoja akifanya kazi yake ipasavyo itawezesha haya makundi maalum kupata sehemu ya Sh.9 trilioni iliyotengwa na Serikali kwa ajili yao kwa mwaka huu,” amesema Maswi.
Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 inaitaka kila taasisi nunuzi kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya mwaka ya ununuzi wa umma kwa ajili ya makundi maalum ambayo ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.