Mtaalamu wa utafiti, Profesa Sam Wang amelazimika kutafuna wadudu katika kipindi kilichorushwa mubashara na kituo cha runinga cha CNN ili kutimiza ahadi aliyoitoa endapo Donald Trump angefikisha alama 240 za majimbo ya uchaguzi.

Profesa Wang ambaye kampuni yake ni miongoni mwa makampuni yaliyofanya utafiti ulioonesha kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Democratic, Hillary Clinton alikuwa na nafasi zaidi ya kushinda uchaguzi huo, aliahidi kuwa endapo matokeo ya uchaguzi yangekuwa tofauti angekula wadudu wasiolika.

Kabla ya kutekeleza ahadi yake, Profesa Wang ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu alionesha kujutia ahadi yake.

“Nadhani kula wadudu kwenyewe kunatutoa katika kufuatilia mambo muhimu ya kisera kama uteuzi katika Mahakama ya Juu,” alisema.

“Kama ilivyokuwa kwa Yohana Mbatizaji akiwa nyikani, alikuwa nzige na asali. Ninajichukulia kama niko nyikani kidogo. Yote kwa yote, nilikosea,” aliongeza.

Profesa huyo ni mmoja kati ya watu maarufu waliotoa ahadi mbalimbali za kushangaza endapo Trump angeshinda uchaguzi.

Mshindi wa tuzo ya Nobel ambaye ni mwandishi maarufu wa vitabu, raia wa Nigeria aishie nchini Marekani, Wole Soyinka aliahidi kuchana kibali cha kuishi nchini humo (green card) kama Trump atashinda uchaguzi wa Marekani. Lakini sasa amesema anasubiri hadi aapishwe.

Trump anatarajiwa kuapishwa rasmi kuwa Rais mpya wa Marekani Januari mwakani.

NATO: Trump sio chaguo la ulaya na Marekani
Clinton: FBI ni tatizo