Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameibukia Kigali, Rwanda na kukanusha taarifa kuwa alijiuzulu nafasi ya Uenyekiti katika hatua za mwisho ili aIhujumu Ukawa.

Akiongea na kituo kimoja cha redio jijini humo, Profesa Lipumba alidai kuwa Ukawa ilipoteza muelekeo wake baada ya kumkaribisha Edward Lowassa ambaye ni kada mkongwe wa CCM kugombea nafasi ya urais kinyume na makubaliano yao ya awali.

Alisema hapo awali viongozi wa Ukawa walikutana na kukubaliana kuwa Dk. Slaa ndiye atakayepewa nafasi ya kugombea urais kupitia umoja huo baada ya kubaini kuwa chama chake kina uwezo wa kifedha wa kuhudumia gharama za uchaguzi tofauti na Chama Cha Wananchi (CUF).

Profesa Lipumba alidai kuwa uamuzi wa mwisho wa kumpa Lowassa nafasi hiyo ni kujichanganya kwa kuwa hivi sasa wagombea wote wa nafasi ya urais ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi.

“Sasa kuna mgombea wa CCM kupitia CCM na mgombea wa CCM kupitia Ukawa. Kwa hiyo wana CCM watachagua mwana CCM kupitia CCM au mwana CCM kupitia Ukawa,” alisisitiza Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba ambaye alikuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa Ukawa, alijiuzulu nafasi yake uenyekiti wa CUF siku chache baada ya kuonekana hadharani akimsafisha Edward Lowassa na kumkaribisha katika umoja huo.

Sammata Na Ulimwengu Kuwakabili Azam FC
Lowassa Adai Akiingia Ikulu Nchi Itatulia ‘Tuli’, Ausuta Uchumi Wa JK