Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona mabadiliko kwenye sekta ya mifugo si tu kwa kijiji cha Msomera bali kwa nchi nzima.
Majaliwa, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Viongozi na wananchi waliohudhuria kikao cha siku moja cha kukabidhi rasmi mradi wa makazi maalum katika kijiji cha Msomera kwa Wilaya za Handeni na Kilindi za Mkoani Tanga.
Amesema, “serikali hii imesema eneo la Msomera litakuwa eneo la mfano kwa ufugaji wa kisasa na wa kibiashara. Kwa hiyo ni lazima tuweke utaratibu wa kufanya lionekane ni eneo la ufugaji wa kisasa.”
Kijiji hicho cha Msomera, kwa sasa ni makazi ya wananchi ambao kuanzia Juni, 2022 walihama kwa hiari toka Hifadhi ya Ngorongoro, ili kulinda ikolojia na uoto wa asili katika eneo hilo ambapo walipewa nyumba za kwenye eneo la ekari 2.5 na la malisho ekari tano.