Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameteungua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu kupisha uchunguzi kutokana na kubaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha katika Mamlaka hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu imeeleza kuwa Rais Magufuli amechukua uamuzi huo leo (Januari 25) baada ya kupata taarifa za matumizi ya shilingi bilioni 179.6 huku kukiwa na malalamiko ya utendaji usioridhisha wa Mamlaka hiyo katika utoaji wa vitambulisho vya Taifa.

“Taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi sasa imetumia Sh.179.6 bilioni. Kiasi hiki ni kikubwa na Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizi zilivyotumika, maana Rais amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa,” imeeleza taarifa hiyo.

Kadhalika, Rais Magufuli amemsimamisha kazi Maimu pamoja na maafisa wengine wanne wa Mamlaka hiyo waliotajwa kwa majina ya Joseph Makani (Mkurugenzi wa TEHAMA), Rahel Maande ( Afisa Ugavi Mkuu), Sabrina Nyoni (Mkurugenzi wa Sheria), George Ntalima (Afisa usafirishaji).

Rais ameagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kufanya ukaguzi katika manunuzi yote ya Mamlaka hiyo, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi kuhusu thamani ya fedha (value for money) kwenye utoaji wa vitambulisho, na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza kama kulikuwa na vitendo vya rushwa.

Katibu Tawala wa Katavi afyekwa na kasi ya Magufuli, Baadhi ya Mabalozi warudishwa nyumbani
Muelekeo Wa Upepo Wa Samatta Wageuka Akiwa Lubumbashi