Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa miradi 26 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.9 huku akisema dhamira ya serikali ni kufikisha maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwasambazia huduma muhimu za umeme na maji.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo Februari 14, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Viongozi na Wadau wa nishati, mara baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba ya miradi ya Uimarishaji Gridi ya Taifa na Umeme Vijijini.
Amesema, ni asilimia 43.9 tu ya vitongoji nchini ndivyo vina huduma ya umeme, na kwamba kazi ya kuwapelekea maendeleo wananchi hasa umeme bado ni kubwa, na kwamba utanufaisha maeneo 336 ya uzalishaji, hivyo ina faida kubwa kwa Watanzania kwa kuwa itahusisha pia migodi midogo, kilimo, vituo vya afya na vyanzo vya maji.
Dkt. Samia amesema mikataba hiyo iliyosainiwa baina ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijinini (REA) pamoja na wakandarasi mbalimbali itasaidia kuondoa kilio kikubwa cha hivi sasa cha Watanzania wengi ambacho ni pamoja na umeme.