Rais wa Visiwa vya Comoro, Azali Assoumani amechaguliwa tena kwa asilimia kubwa ya kura zilizopigwa, kulingana na matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.

Ushindi huo umetokea wakati uchaguzi wa nchi hiyo umeripotiwa kuwa na utata na kusababisha hali ya wasiwasi, ambapo wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakidai kuwepo na udanganyifu katika kuhesabu kura.

Azali, aliyeingia madarakani mwaka 2016, amepata asilimia 60.77 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa Machi 24 mwaka huu, akifuatiwa na mgombea wa chama cha JUWA katika kinyang’anyiro hicho Mahamoudou Ahamada, aliyepata asilimia 14.62.

Aidha, Azali mwenye umri wa miaka 66, ataanza mhula mpya wa miaka mitano katika visiwa vya Comoros, vyenye wakazi 800,000, katika moja ya nchi maskini zaidi duniani na yenye misukosuko ya kisiasa.

Zoezi la uhesabuji kura ilikabiliwa na vurugu, ambapo maafisa wa usalama walivunja maandamano ya upinzani kwa nguvu, ingawa Rais Azali amekiri kuwepo kwa dosari, na ametaka nchi hiyo kuangazia umoja na ujenzi wa taifa.

“Ni kweli kwamba kulikuwepo na mapungufu madogo madogo, lakini tunafuraha kwamba mambo hayakuwa mabaya sana, tunajipongeza wenyewe, tunamshukuru Mungu na watu wa Comoros. lakini nilivyosema, yale tumefanya ndio rahisi, wakati mgumu sasa ni kujenga nchi na nahitaji mchango wa kila mtu.”amesema Rais Azali

Hata hivyo, wanasiasa kutoka vyama vya upinzani wamedai kuwa dosari zilizojitokeza wakati wa kuhesabu kura na zilizoripotiwa na tume ya uchaguzi ndizo zilizompa ushindi Rais Azali, hivyo wametaka matokeo hayo yatenguliwe.

 

Manchester United yampa Solskjaer mkataba wa kudumu
Serikali ilirekebisha sheria ya madini ili kuimarisha usimamizi- Biteko