Wakati Kundi la Kwanza la Wachezaji wa Simba SC likiwasili salama mjini Casablanca nchini Morocco, Kocha Mkuu wa klabu hiyo Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema, anatarajia kuwapa kazi maalum Washambuliaji wake wawili Jean Baleke na Kibu Denis ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya dhidi ya Raja Casablanca.

Simba SC ambayo tayari imefuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Jumamosi (Aprili Mosi) inatarajiwa kuvaana na Raja Casablanca, ukiwa ni mchezo wa mwisho wa Kundi C utakaochezwa nchini Morocco.

Robertinho amesema: “Ni jambo zuri kuuendea mchezo huu tukiwa tayari tumeshafuzu Robo Fainali kwani hii itatupunguzia presha ya mchezo, lakini hatutauchukulia kama mchezo rahisi, bali tutacheza kwa kuwaheshimu wapinzani na kusaka mabao.”

“Mchezo wetu uliopita tulikuwa na uwiano mzuri kwenye nafasi ya ushambuliaji hususani Kibu Denis na Jean Baleke, natarajia kuona wanafanya vizuri zaidi kwenye mchezo huu.”

Mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Februari 18, mwaka huu, Simba SC ilipoteza dhidi ya Raja Casablanca kwa mabao 0-3.

Kocha Young Africans atoa ahadi nzito DR Congo
Singida Big Stars wanautaka ubingwa