Rufaa ya kupinga hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi iliyomwachia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake imepangwa kuendelea kusikilizwa Desemba 28, 2022.

Leo Desemba 21, 2022 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilipanga kutaja rufaa hiyo namba 155/2022 ambapo imetajwa mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Judith Kamala.

Muomba rufaa katika shauri hilo aliwakilishwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Akisa Mhando, huku Sabaya akiwakilishwa na wakili Fauzia Mustafa.

Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya, akizungumza na wakili wake Fauzia Mustafa

Aidha, upande wa waomba rufaa umeomba Mahakama hiyo kutoa kwa mara ya pili matangazo ya hati ya wito kwa wajibu rufaa wanne katika rufaa hiyo baada ya wajibu rufaa hao kutofika mahakamani.

Hata hivyo, Sabaya amefika mahakamani leo peke yake, huku wajibu rufaa wengine ambao ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya wakikosekana.

Itakumbukwa kuwa desemba 14, 2022 Jaji Salma Maghimbi, anayesikiliza rufaa hiyo aliiahirisha na kutoa amri kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kuchapisha kwenye magazeti tangazo la hati wito kwa wajibu rufaa wanne kwenye rufaa hiyo.

Wakili Akisa aliieleza mahakama kuwa shauri hilo limepangwa kwa ajili ya kutajwa ambapo aliomba kufahamu iwapo hati za wito kwa wajibu rufaa ambao hawapo mahakamani zimetolewa kwenye magazeti kama ilivyokuwa ameagizwa mara ya mwisho.

Naibu Msajili huyo alieleza hati hizo za wito zimetolewa kwenye magazeti mawili ambayo ni Mwananchi la Desemba 17, 2022 na The Citizen la Desemba 20, 2022.

“Kwa kuwa imeshatangazwa na hawajaja mahakamani tunaomba mahakama itangaze kwa mara ya pili kisha tupatiwe tarehe ya mwisho kuona kama wamepata tangazo hilo au la ili tuombe necessary orders,tunaomba itajwe Desemba 28,” amesema Wakili Akisa

Naibu Msajili huyo aliahirisha rufaa hiyo hadi Desemba 28, 2022 itakapoendelea kusikilizwa.

NIDA kutoa vitambulisho kwa mfumo wa mtandao
‘Pita huku’ yamfikisha Makabila BASATA