Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Innocent Bashungwa amezitaka taasisi binafsi kuchangamkia fursa zinazotokana na maonesho ya nne ya viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Ameyasema hayo leo, Agosti 5, 2019 jijini Dar es salaam, wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo ambapo amewataka wadau katika sekta binafsi kujitengenezea mtandao mzuri kwa ajili ya kuzitumia vyema fursa zinazojitokeza.
Bashungwa ameongeza kuwa jumla ya washiriki 3,100 kutoka nchi wanachama wa SADC wanashiriki katika maonesho hayo. Ameyaelezea kuwa ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa ndani ya nchi kupanua wigo wa biashara zao na kukutana na wafanyabiashara kutoka mataifa mengine.
Amesema kuwa kwasasa Serikali inaendelea kuwahamasisha wananchi kuchangamkia fursa hizo ambazo kwa juma hili la maonesho ya SADC zitaweza kuwanufaisha katika kuwajengea misingi bora zaidi ya kibiashara.
Aidha, ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika biashara ndani ya SADC ambapo kwa mwaka 2018 mauzo yalikuwa $999.64 Milioni, ikilinganishwa na mauzo ya $877.8 Milioni kwa mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 21.16.
“Mwaka huu tumepata heshima kubwa ya kuwa waandaaji wa maonesho ya nne ya viwanda ya jumuiya ya SADC, hivyo basi naziomba sekta binafsi zichangamkie fursa hii ambayo itaweza kuwajengea mtandao mkubwa wa kufanya biashara,” alisema.
“Maonyesho haya ni fursa kubwa kwetu hasa katika nyanja ya uchumi,” aliongeza Bashungwa.
Bashunwa alisisitiza kuwa nchi wanachama wa jumuiya ya SADC zimewekeza nguvu kubwa katika ukuzaji viwanda, uendelezaji biashara na uzalishaji ajira ndani ya jumuiya hiyo.
Kauli Mbiu ya Mkuano wa SADC unaofanyika jijini Dar es Salaam mwezi huu ni “Mazingira Wezeshi ya Kibiashara kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda.” Kauli mbiu hiyo inaakisi kauli mbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda’ inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Magufuli.