Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametumia kikao cha Baraza la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, kuomba kuungwa mkono katika kinyang’anyiro cha Tanzania kuwa mwenyeji wa Taasisi ya Uthibiti wa Dawa ya Umoja wa Afrika (AMA ) ikifuatiwa na Nchi ya Namibia, Zimbambwe.
Aidha Baraza la SADC, limepitisha rasmi bajeti kwa ajili ya kuhakikisha Kiswahili kinatumika katika ngazi zote za vikao vya SADC ikiwa ni pamoja na kutafsiri Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo kwa lugha ya Kiswahili tofauti na awali ambapo Kiswahili kilitumika wakati wa mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali pekee.
Uamuzi wa Baraza hilo la Mawaziri wa SADC umefikiwa katika siku ya pili ya kikao cha Bazara kinachoendelea Lilongwe Nchini Malawi kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Baraza la Mawaziri wa SADC, wamepata fursa pia ya kupitia majina yanayopendekezwa kwa ajili ya kumpata Katibu Mtendaji mpya wa Jumuiya hiyo kutokana na Katibu Mtendaji aliyepo hivi sasa Dkt. Stergomena Tax kumaliza muda wake katika Jumuiya hiyo.
Hata hivyo jukumu hilo la kumpata Katibu Mtendaji mpya wa SADC limeachwa mikononi mwa Wakuu wa Nchi na Serikali ambao watakutana Agosti 17 na 18, 2021 Lililongwe Nchini Malawi, ambapo watapitisha jina moja kati ya mawili yaliyowasilishwa kutoka katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC na Botswana.
Mkutano huu wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaofanyika Lilongwe Nchini Malawi utakuwa ni Mkutano wa mwisho wa Katibu Mkuu Mtendaji aliyepo hivi sasa Dkt. Stergomena Tax anayemaliza muda wake wa miaka nane.