Mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti walizaliwa eneo la Ikonda, wilaya ya Makete Tanzania mwaka 1996 na kuanza masomo yao katika shule ya msingi ya Ikonda kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Maria Consolata na baadaye kidato cha sita katika shule ya Udzungwa wilaya ya Kilolo.

Baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita Septemba mwaka jana, walijiunga na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, Mkoani Iringa.

Desemba, 2017 walianza kuugua maradhi ya moyo na wakahamishiwa katika taasisi ya maradhi ya moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako walilazwa kwa miezi miwili.

swahili

Mapacha hao walioungana mara baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita walikuwa wenye furaha sana na walieleza furaha yao kueleza ndoto zao.

“Tulipokea matokeo yetu tukiwa kwenye mazingira ya nyumbani tu, tukiendelea na shughuli zetu za kila siku, tukaambiwa matokeo yametoka na tumefanya vizuri, tulikuwa tukiwaza kabla ya hapo, unajua kwenye mitihani ya mwisho huwezi kujiamini sana,” walisema mapacha hao.

Maria na Consolata walichagua chuo kikuu cha Ruaha ambapo walieleza sababu za kuchagua chuo hicho kuwa wanapenda sana mazingira ya Iringa kwani hali yake ya hewa ya baridi wameshaizoea pia wasingependa kuishi mbali na walezi wao ambao ni Masista.

“Kwanza tunapenda mazingira ya Iringa, hatukutaka kwenda Dar es Salaam kwa sababu ya kwanza tunapenda kuishi pamoja na walezi wetu Masista waliokuwa wanatulea tukiwa wadogo na pili mikoa mingine ni mbali na tunapoishi. Pia ni kwa sababu kwa hali yetu tulivyo hatumudu kuishi kwenye mazingira ya joto. Mji wa Iringa ni baridi, hali hii tumeizoea.”

Pamoja na hayo yote, Maria na Consolata wamekuwa na jicho la tofauti kwani pamoja na walivyo wamekuwa wenye mawazo chanya muda wote huku wakitoa ushauri kwa wazazi kwa kuwahimiza kuwajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu wakisema hakuna lisilowezekana.

“Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na mtoto mlemavu ni laana.”

Wamewahimiza wazazi wawapende watoto walemavu na wawaone kama watoto wengine na kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kulitumikia Taifa kwa moyo wote.

Kifo cha Maria na Consolata kimewagusa watu wengi, ambapo moja wapo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye miezi kadha alikutana na pacha hao.

Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa Twitter ameeleza kusikitishwa kwake na vifo vyao.

“Nimesikitishwa na kifo cha Maria na Consolata. Nilipokwenda hospitali waliliombea Taifa. Walikuwa na ndoto ya kulitumikia Taifa. Poleni familia, Masista wa Maria Consolata na wote walioguswa, pumzikeni mahali pema wanangu. BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE.” ameeleza Rais Magufuli.

Pacha hao hadi kufariki kwao walikuwa na umri wa miaka 22 na wamekuwa wakitunzwa na Masista wa Kanisa Katoliki tangu walipokuwa wadogo.

Safari ya Maria na Consolata hapa Duniani imekamilika na huku wakiuacha upweke mkubwa kwa walezi wao lakini pia watanzania wote waliokuwa wakiguswa na maisha yao.

Maria na Consolata wameacha funzo kubwa sana kwa wazazi na watu wote, na huenda hiyo pekee ilikuwa kazi yao duniani na wameikamilisha, kwani kupitia wao tumeona umuhimu wa kuwapenda na kuwajali watoto wote katika usawa kwani kila mtu akiwezeshwa anaweza kuishangaza dunia kwa kufanya mambo makubwa na yenye tija katika jamii.

Tumeshuhudia wakifanya vizuri katika masomo yao lakini wenye ndoto kubwa sana, wamekuwa wakiwaasa wazazi kuwapenda watoto wenye ulemavu kwa upendo wa dhati bila kukata tamaa wala kuwanyanyapaa.

“Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na mtoto mlemavu ni laana. Pili wawaone kama watoto wengine na kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.” wamesema mapacha hao.

Hii ni tosha kuwa ni fundisho kubwa sana walilotuacha Maria na Consolata katika safari yao Duniani, ndiyo maana nathubutu kusema kazi yao wameimaliza na Mungu awapumzishe kwa amani.

Baba mzazi amuua mwanae kwa Panga Saa chache kabla ya harusi
Maneno ya Rais Magufuli baada ya kupata taarifa za msiba wa mapacha walioungana Maria na Consolata