Baraza la Seneti la Marekani linatarajiwa kukutana leo Ijumaa kupiga kura ya kumuidhinisha Jenerali mstaafu, Lloyd Austin aliependekezwa na Rais Joe Biden kwenye wadhifa wa Waziri wa Ulinzi.
Jana Alhamisi Baraza la Wawakilishi na Seneti walipitisha kanuni ya kisheria kumruhusu Austin kuchukua wadhifa wa Waziri wa Ulinzi kama raia wa kawaida ikiwa ni chini ya miaka 7 tangu ajiuzulu kwenye jeshi la Marekani.
Austin ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Vikosi vya Marekani Mashariki ya Kati na Asia kusini na Kamanda wa Uongozi wa jeshi, akiidhinishwa na Seneti, atakuwa Mmarekani mweusi wa kwanza kuchukua wadhifa wa Waziri wa Ulinzi.
Baraza la Seneti linatarijiwa pia kumuidhinisha Balozi wa zamani William Burns aliependekezwa na Rais Biden kuongoza idara ya Ujasusi ya Marekani, CIA.