Serikali nchini, imesema itashirikisha wananchi kuhusu utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri ya kukiondoa Kijiji cha Ngaresero katika Pori Tengefu la Ziwa Natron, kutokana na Pori hilo kuwa ni moja kati ya maeneo yaliyotolewa maelekezo na Baraza la Mawaziri kuwa lipandishwe hadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Emmanuel Lekishon Shangai, lililoulizwa na Zaytun Swai.
Katika swali hilo, Mbunge Lekishon alitaka kujua nilini Serikali itaondoa Kijiji cha Ngaresero kwenye eneo la Pori Tengefu la Pololet, baada ya kujumuishwa kimakosa ambapo ufafanuzi ulisema sheria ya ardhi na. 4 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2019, ardhi ya Pori Tengefu Ziwa Natron ipo kwenye ardhi ya Hifadhi.
Aidha, Masanja pia alibainisha kuwa Serikali itashughulikia mgogoro huo kwa kukutana na wananchi, ili kufikia muafaka na hatimaye pori hilo liwe na hadhi iliyotarajiwa kama ambavyo ilipendekezwa awali na Baraza la Mawaziri.