Wizara ya Afya kwa kushirikiana Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau wa Sekta ya Afya, inatarajia kuendesha Kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio kwa watoto zaidi ya Milioni 3,250,598 walio chini ya miaka 8 kwenye Mkoa wa Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu hii leo Septemba 8, 2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio, ambayo inatarajiwa kuanza kufanyika nchini kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2023.
Amesema, “nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa tutakuwa na Kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya Polio kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka nane na Kampeni hii itafanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 21 – 24, 2023 katika Mikoa hiyo sita inayopakana na nchi zenye mlipuko wa Polio.”
Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa Mkoa wa Rukwa Wanatarajia kufikia watoto 391,883 Kagera 729,387 Kigoma 884,477 Mbeya 614,346 Katavi 227,862 na Songwe 402,643 na kudai kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuifikia idadi hiyo ya watoto ili kuwakinga dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili kinachoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.
Hata hivyo, amesema Tanzania inaendesha Kampeni hiyo ya chanjo kutokana na Wizara Mei 26, 2023 kupokea taarifa za uwepo wa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja ambaye alionyesha dalili za kupooza kwa ghafla kutoka Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa na uchunguzi wa Maabara ulithibitisha kuwa ana maambukizi.
“Maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Polio yametolewa taarifa pia katika nchi zinazopakana na Tanzania mfano Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia hivyo hali hii inaongeza tishio na hatari ya maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Polio kwa nchi yetu hususani katika Mikoa inayopakana moja kwa moja na nchi hizo,” amesema Ummy.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu amesema katika kuendeleza mikakati ya kutoa chanjo dhidi ya Polio, wametoa hamasa kwa wazazi kuhakikisha wanawatoa watoto wao kupata chanjo hii ili kuwaepusha watoto kupata ulemavu ambao kwakweli unakingika kwa kutumia Chanjo.