Athari kubwa za kiafya kwa binadamu pamoja na mazingira zitokanazo na matumizi ya Zebaki bado ni tatizo nchini na Serikali imekuwa ikiwaasa maafisa mazingira na wakaguzi wa migodi kuwa waadilifu ili kutimiza azma ya Serikali ya kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu.
Naibu Katibu Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama ameyasema hayo wakati akifungua Warsha ya mafunzo ya siku mbili kwa Wakaguzi wa mazingira na migodi kuhusu utekelezaji wa mpango kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya ZEBAKI kwa wachimbaji wadogo wa Dhahabu, anasema matumizi ya Zebaki yana madhara ya kiafya na mazingira kiujumla.
Amesema, “hatua hii imekuwa ikitekelezwa na kuendelea kutiliwa mkazo na ndio mana bado Wakaguzi wa mazingira na migodi wanatakiwa kuwa waadilifu na kujiepusha na Vitendo vya Rushwa wakati wakitekeleza mpango kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi hayo ya ZEBAKI kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu.”
Naye Mkurugenzi wa Uzingatiaji na utekelezaji wa sheria Baraza la Taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira – NEMC, Redempta Samuel amesema malengo ya mafunzo hayo ni kuwapatia elimu wakaguzi hao pamoja na kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Baadhi ya washiriki wakiongea wakati wa warsha hiyo, wamesema mafunzo hayo yanafaida kubwa kwao Kwani yatawasaidia katika utendaji wao wa Kazi katika kupunguza matumizi ya zebaki migodini kwa wachimbaji wadogo wa Dhahabu.
Oktoba 10, 2013 Tanzania ilisaini Mkataba wa Minamata kuhusu matumizi ya zebaki ukiwa na lengo la kupunguza matumizi ya kemikali hiyo yenye athari kwa afya na mazingira na wakaguzi wa mazingira wanaaswa kuwa waadilifu katika shughuli zao ili kupunguza matumizi ya zebaki.