Katika kuhakikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaendelea kudumu na kuimarika, Serikali imesema inaendelea na jitihada za kuzitafutia ufumbuzi Hoja nne za Muungano zilizobaki.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Khamis Juwakali.
Pinda alisema, kuwa miongoni mwa hoja zilizobaki ni pamoja na Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Usajili wa Vyombo vya Moto na Uingizaji wa sukari inayozalishwa Zanzibar katika Soko la Tanzania Bara na kuzitaja changamoto nyingine kuwa ni Mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu.
Aidha, ameongeza kuwa kwa msingi huo wizara zinazohusiana na masuala ya Muungano hukutana kwa ajili ya kujadili changamoto zinazokabili sekta zao na kuzitafutia ufumbuzi na ikimbukwe kuwa Desemba 6, 2022 jumla ya hoja nne zilipatiwa ufumbuzi katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na SMZ kilichofanyika jijini Dodoma.
Hoja zilizopatiwa ufumbuzi katika kikao hicho ni pamoja na Malalamiko ya Wafanyabiashara wa Tanzania Zanzibar kutozwa kodi mara mbili wanapoagiza mizigo kutoka nje ya nchi na kupeleka Tanzania Bara, Kodi ya Mapato na Kodi ya Zuio.
Zingine ni Ongezeko la Gharama za Umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO pamoja na Hoja ya Mkataba wa Mkopo wa Fedha za Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (Terminal III).