Serikali imelipa madeni ya wazabuni, wakandarasi na malimbikizo ya wafanyakazi yanayofikia kiasi cha shilingi bilioni 190 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu baada ya kufanya uhakiki wa madeni halali inayodaiwa na wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji wakati akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa mkoa wa Kagera akiwa katika ziara ya kikazi kukagua utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).

Amesema kuwa wazabuni wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 67.2, wakandarasi wamelipwa shilingi bililioni 24.2, watoa huduma mbalimbali wamelipwa Shilingi bilioni 38, watumishi wa umma wamelipwa Shilingi bilioni 37, huku wadai wengine wakilipwa shilingi bilioni 24.

Aidha, amesema kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi trilioni 1 kwa ajili ya kulipa madeni mbalimbali na kwamba itaendelea kulipa madeni yote yaliyohakikiwa.

Vile vile Dkt. Kijaji ameiambia Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera kuwa Serikali inatambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa kutokana na kulipa kodi zinazochangia kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za jamii.

Akizungumza kwa Niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro, amewashauri wafanyabiashara hao kupanua wigo wa biashara zao ili waweze kunufaika na uwepo wa soko huru katika nchi zaidi ya nne zinazopakana na mkoa huo ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, DRC Kongo, Kenya na nchi nyingine.

Liverpool yaishushia Maribor kipigo cha mwizi, Spurs, Madrid hakuna mbabe
Video: Video ya Lissu yazua gumzo, Nassari aivimbia Takukuru