Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere, ilisema Bohari ya Dawa (MSD) imeonesha madhaifu na mapungufu ikiwemo kwenye matumizi ya pesa, manunuzi pamoja na namna taasisi hiyo inavyojihusisha na mashirika ya umma.

Ripoti hiyo ya CAG aliendelea kutanabaisha kuwa taasisi hiyo inashindwa kwa asilimia 66 kutimiza mahitaji ya bidhaa za dawa na vifaatiba kwa wateja, ununuzi usiozingatia sheria pamoja na kuwepo kwa mikataba iliyosainiwa bila kupekuliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ripoti hiyo ya CAG ilibaini kuwa taasisi hiyo ya umma ilitumia jumla ya Sh215.99 milioni kulipa watumishi watatu posho ya kujikimu walipokwenda China.

CAG Kichere aliednelea kuwasomea waandishi wa habari kuwa alibaini barua yenye Kumb. Na. CEA.169/178/03/18 ya Oktoba 13, 2020 ya uteuzi wa maofisa watatu kwenda China kwa ajili ya kutafuta watengenezaji ili kusambaza mashine 71 za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo ‘hemodialysis’ na kutoa ushauri kwa Serikali juu ya ununuzi wa mashine hizo na kuongeza kuwa mchakato huo haukuhusisha kitengo cha usimamizi wa ununuzi na bodi ya zabuni, bali mchakato mzima ulifanywa na watu watatu wakiwa China kwa Sh2.79 bilioni.

“Nilibaini kuwa, ili kuwezesha ununuzi wa mashine hizo, MSD ilitumia Sh215.99 milioni kulipa watumishi watatu posho ya kujikimu kwa siku 61 pamoja na gharama za usafiri kwenda China kwa madhumuni ya mazungumzo na kutafuta viwanda. Nina shaka na mchakato mzima wa ununuzi na matumizi ya fedha za umma,” alisema Kichere

Kichere alieleza kuchelewa kuanza uzalishaji kwa viwanda vinavyomilikiwa na mashirika ya umma huku akigusia uanzishwaji wa kiwanda cha kutengeneza glovu bila kufanya upembuzi yakinifu wa kibiashara hiyo ikiwa ni katika ripoti ya mapitio ya uwekezaji katika mashirika ya umma

CAG Charles Kichere

CAG alibaini ripoti ya upembuzi yakinifu ya MSD ya Septemba 2020 juu ya kuanzishwa kwa eneo hilo la viwanda haikujumuisha mchanganuo wa biashara pamoja na mpango wa kina ulioandaliwa ili kupata hoja za kuanzisha mradi na kutathmini faida, gharama na vihatarishi vya biashara.

Alisema baada ya kupitia muhtasari wa mkutano wa 157 wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, iliibua wasiwasi wa upembuzi yakinifu na kuiagiza taasisi hiyo kueleza kwa uwazi uwezo wao katika masuala ya fedha, utaalamu, teknolojia na kuonyesha chanzo cha asilimia 10 ya malighafi kwa ajili ya uzalishaji kutoka vyanzo vya ndani.

Katika ripoti hiyo, Kichere alisema taasisi hiyo ilifanya ununuzi wa bidhaa bila mikataba wenye thamani ya Sh9.90 bilioni na Dola 1.42 milioni za Marekani kinyume na kanuni ya 233(1) (2) na kanuni ya 75 ya kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013.

Katika hatua nyingine, CAG amebaini mikataba yenye thamani Sh17.92 bilioni iliyotolewa na kusainiwa bila kupekuliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kinyume na kanuni ya 59 (1)(2) na kanuni ya 2 ya kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013.

Hata hivyo, CAG Kichere alisema katika ukaguzi wa ununuzi alibaini utekelezaji wa mikataba sita ya ununuzi ya Sh43.98 bilioni katika bohari hiyo ambayo haikuwa katika bajeti wala kujumuishwa katika mpango wa ununuzi wa mwaka.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan aliitaka Bohari hiyo ya Dawa kujitathmini kuanzia kwee utendaji pamoja na uongozi mzima ambapo alisema kuwa MSD imekua ikishindwa kutekeleza majukumu yake kuendana na mahitaji ya Jamii.

Aprili 14, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi na kumteua Rosemary William Slaa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bohari ya Dawa (MSD).

Sayari 4 kuonekana angani April
KMC FC kukipiga na Kagera Sugar saa tatu usiku Kaitaba