Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameshiriki hafla ya ugawaji majiko Banifu 114 yaliyotolewa na Jumuiya ya Wanawake ya Wakala wa Nishati Vijijini, yanayotumia nishati safi na salama yakupikia katika Kijiji cha Zanka na Kigwe, Wilayani Bahi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.
Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo, Senyamule amesema matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa chanzo kikuu kinachotumika kwa kupikia hasa maeneo ya Vijijini na kupelekea uwepo wa athari katika mazingira na afya ya Binadamu.
Amesema, “Serikali itaendelea kuweka vivutio kwa wazalishaji na wasambazaji wa Teknolojia na bidhaa za nishati safi na salama ya kupikia na kuongeza wigo wa upatikanaji wa bidhaa pamoja na kutoa unafuu wa gharama ili kuwezesha watumiaji kutumia bidhaa hiyo.”
Amesema, zaidi ya tani milioni mbili za Mkaa zimekuwa zikitumika kwa mwaka kama nishati ya kupikia hivyo imeleta athari za mazingira na afya katika jamii, zaidi ya asilimia 85 ya kaya hapa nchini hutumia kuni na Mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Uendelezaji Masoko na Teknolojia Wakala wa Nishati Vijijini – REA, Advera Mwijage amesema jiko hilo linatumia nishati mbili ambayo kuni na linaweza kutumika sehemu yoyote kwa kumsaidia mwananchi kupunguza matumizi ya fedha na ukataji wa miti ovyo.
Awali, Mwenyekiti wa kijiji cha Kigwe, Jeremia Sobayi alisema kila mwananchi anatakiwa kuwa balozi mzuri katika matumizi sahihi ya majiko hayo, na kuwa mlinzi wa mwenzake ili yasitumike kufanya matumizi nje ya malengo.