Mtendaji Mkuu wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC, Barbara Gonzalez amesema malengo ya Klabu hiyo kwa sasa, ni kumuajiri kocha kutoka Barani Afrika ili kuziba nafasi ya Didier Gomes ambaye aliondoka klabuni hapo juma lililopita.

Inaelezwa kuwa Uongozi wa Simba SC, umeshaanza mzungumzo ya kumuajiri Kocha Msaidizi wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Rulani Mokwena kuwa Kocha Mkuu wa kikosi chao.

Barbara amesema Uongozi wa Simba SC unaendelea kufanya mchakato wa kumpata kocha bora atakayekinoa kikosi chao, baada ya kuondoka kwa Gomes, hivyo wanachama na mashabiki wanapaswa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki.

“Suala la kocha halihitaji kukurupuka, kwani tunaweza kumpata mwenye wasifu mkubwa lakini akashindwa kutibu matatizo yaliyopo katika kikosi cha Simba na shida ikabaki pale pale,”

“Kama atakuwa Mokwena au mwingine hilo litajulikana ndani ya muda mfupi, lakini malengo ya klabu ni kumpata kocha kutoka Afrika na si Mzungu kama iliyetoka”

“Tunaweza kumpata kocha wa Afrika ambaye tunamuhitaji na wasifu wake usiwe mkubwa na akaweza kuisaidia timu kufikia malengo yake kwani atakuwa na kiu ya mafanikio na tutadumu naye kwa muda mrefu”

“Angalia klabu kama Chelsea wakati wanamchukua Thomas Tuchel wengi hawakuwa na imani naye, ila baada ya muda mfupi ameifanya timu kucheza vizuri na kushinda ubingwa wa Ulaya.” Amesema Barbara.

Simba SC imeripotiwa kupokea maombi ya makocha zaidi ya 70, siku chache baada ya kuachana na Kocha Didier Gomes kufuatia kushindwa kufikia lengo la kutonga hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika 2021/22.

Namungo FC yawasili Dar, kukabili Simba SC jumatano
Simulizi: Penzi la Dada yangu wa Tumbo moja lilivyonisahaulisha kuoa