Baada ya timu kongwe za Simba na Yanga kufungiwa na Serikali kutumia Uwanja wa Taifa kutokana na vurugu za mashabiki wao walizofanya Oktoba mosi vigogo hao wa soka nchini wamesema hata Uwanja wa Uhuru ‘Shamba la bibi’ upo safi.

Timu hizo zimehamia Uwanja huo wenye nyasi bandia ambapo awali waliukataa kutokana na kusababisha majeruhi kwa wachezaji wao na Simba waliliandikia barua Shirikisho la soka nchini TFF kuupinga kutokana na uchakavu wa eneo la kuchezea lakini baada ya kupigwa marufuku kutumia Uwanja wa Taifa, hawana chaguo mbadala, zaidi ya kukubali kurejea uwanjani hapo.

Meneja wa Simba Mussa Mgosi amesema kwa sasa hawachagui Uwanja, wapo tayari kucheza popote kwa vile mikoani kuna viwanja vibovu kuliko hata Uwanja wa Uhuru.

“Sisi popote pale tunacheza hata wakitupeleka Karume tupo tayari kikubwa ni kuhakikisha tunashinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuchukua ubingwa msimu huu,” alisema Mgosi.

Mgosi aliongeza kuwa Wekundu hao wanaoongoza ligi wakiwa na pointi 23 wameingia kambini jana kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wao dhidi ya Mbao FC utakaopigwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru baada ya mwishoni mwa juma kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa upande wao Yanga kupitia kwa Kocha wao msaidizi Juma Mwambusi alisema wapo tayari kucheza Uwanja wowote watakaopangiwa kucheza na hawahofii chochote kwa kuwa wana kikosi bora chenye uwezo wa kucheza na timu yoyote nchini, kwa hiyo suala la Uwanja wa Uhuru haliwaumizi kichwa.

“Uwanja wa Uhuru sio mbaya na kwavile ndiyo tumepangiwa kuutumia basi hatuna jinsi na hata ingekuwa sehemu nyingine tupo tayari kikubwa ni kuibuka na pointi tatu, tumejipanga kupambana popote,” alisema Mwambusi.

Video: Mtoto mwenye kipaji atua ofisi za Mkuu wa Mkoa, azidi kuonyesha ubora wake
Nyasi Bandia Za Nyamagana Zawasili TFF