Wakati fulani Marehemu Mjomba wangu, Samuel Makasi (RIP) aliwahi kunipa simulizi moja kuhusu Mataifa mawili yaliyokuwa yakitunishiana misuli kwa zana za kivita na teknolojia. Sina hakika kama simulizi hii ilikuwa ya kweli maana mjomba ni kweli watu walikuwa wakimuamini kwa simulizi za vijimkasa vyake ila mimi nilikuwa namshtukia nahisi kama ananiingiza mkenge, ila zilikuwa zinafundisha mambo mengi ya kimaisha.
Katika simulizi yake alidai kwamba Marekani na Urusi waliingia katika mvutano wakishindana kwenda mwezini, inasemekana Wamarekani walipokwenda mwezini kwa mara ya kwanza walitumia kalamu za wino za kawaida, ili kuandikia utafiti wao wakiwa mwezini lakini jambo la ajabu ni kwamba walipofika kule, kalamu zile zilishindwa kuandika kwa sababu wino ulikuwa unapanda juu kutokana na nguvu ya uvutano wa Mwezini.
Mjomba alisema kwamba jambo hilo liliwakwamisha kurudi na taarifa za utafiti wao, hivyo ilibidi wanasayansi wakae chini na kubuni wino ambao utaendana nauvutano huo wa mwezini ambao ungesaidia wino kutopanda juu wakifika eneo la tukio na utafiti huo ulichukua muda mrefu kufanikiwa kutengeneza wino huo.
Anadai kwamba, wakati Wamarekani wakitumia muda mrefu kutafiti kalamu ya wino ya kwenda nayo mwezini, Warusi wao walitumia muda huo kufanya safari kadhaa mwezini na kurudi na machapisho ya utafiti wao kwa amani, jambo ambalo liliwashangaza Wamarekani kwamba Warusi wamewezaje kufanya utafiti na kufanikisha kuandika kule mwezini kirahisi namna ile?.
Hapa na mimi nilijiuliza pia wamewezaje na sina shaka hata wewe msomaji unajiuliza walitumia mbinu gani, ambayo Mmarekani tunayemfahamu, mbishi asiyependa kushindwa kwa kila jambo katika ulimwengu huu wa kiteknolojia, kapitwa wapi na Mrusi ambaye mara nyingi hufanya mambo yake bila kelele, je? kafanyaje fanyaje Mrusi (hapa Watu wa matukio wangesema, “WE MISO MISONDO UMEPIGAJE HAPO?”).
Mjomba anasema, ukweli ni kwamba wakati Wamarekani wakihangaika kutafiti kalamu za wino za kwenda nazo Mwezini, Warusi wao walikuwa wakitumia Kalamu ya Risasi (Penseli), kuandikia ripoti za tafiti zao, yaani wala hawakuhangaika walitumia akili ndogo sana ya kufanikisha jambo lao kwa kutumia Klamu ya Risasi, bila shaka inashangaza ee.
Mambo kama haya yapo kwenye maisha yetu, mfano katika usafiri wa umma maarufu kama Daladala, humu huwa kuna ladha za pekee za sisi watu wa uchumi wa chini bila kutarajia na wakati wowote usiotabirika huwa unazuka ugomvi ama mabishano, mfano Konda anaweza jibizana na abiria kwa ukali kisa chenchi, yaani Konda anasema hajapata chenchi na abiria anadai apewe chake ili awaze mambo mengine, huwa hapatoshi.
Yanayotokea mengine huwa yanachekesha, yanaudhi, yanafurahisha, yanatafakarisha na hata kukasirisha pia, kwani ukituliza kichwa ukawaza kwa kina unaweza usipate chanzo hasa cha mabishano mpaka kufikia watu kutoleana maneno ya kasfha tena mbele ya kadamnasi kwa jambo linalohitaji busara kidogo tu mkaelewana.
Siku moja niliwahi sikia mabishano kwenye daladala, “Fungua tupate hewa”…. mwingine anajibu “me naloana sifungui kwani Dirisha ni hili pekee kafungue jingine,” kama ujuavyo tena ushuhuda mbele nikapepesa macho yakafika mahala husika naona vuta nikuvute, aliyesimama akifungua dirisha na aliyekaa akilifunga mmoja kijitetea kupata hewa safi mwingine akikataa kuloana na Mvua iliyokuwa ikinyesha na matone yake kupenya ndani ya Gari.
Zoezi hili liliendelea mpaka pale Konda alipoingilia kati, kwanza Konda alihoji endapo wakivunja Kioo wanaweza kuyajenga wakalipa, wagomvi wale wote wakaangaliana kisha wakatulia huku wakitweta kwa mihemo maana ilikuwa ni zoezi zito kwao kwa muda ule na mazingira husika, mara kuna sauti ikasikika, “Jamani hatujawahi kusikia mtu kafa kwa kuloana na maji, watu hufa kwa kukosa hewa.”
Nilivutika sana na sauti hii nikataka kuona ni nani huyu. Shuhuda mimi nikapepesa tena macho sasa mfumo wa ukaaji ukaninyima kuona sura maana naona kichwa, lakini pia nikawa nahisi tu huenda ni yule au huyu kwani kiti wamekaa watu wawili na wote ni wa jinsia moja sasa nani ametoa kauli ile yenye mashiko? sikupata jibu la uhalisia.
Wakati nashika hamsini zangu nikasikia tena Konda kajibu, “Mama waambie hawaelewagi mpaka yawakute,” nikatazama tena kwa umakini, akasimama Mama wa makamo akiomba kushushwa kituo kinachofuata huku akisema, “Maradhi ni mengi wanangu tena maambukizi ya hewa ni zaidi, kuna Uviko hatuna uhakika kama umeisha, kuna Kifua kikuu, kuna mengi wanangu hewa ni kila kitu.”
“Muache Bi. Mkubwa,”…. ilikuwa ni sauti ya Konda akimpa ishara Dereva asimamishe gari ili mama yule ashuke naye akatii, mara baada ya kushuka safari ikaendelea. Utulivu ukafuata lakini dakika moja baadaye Konda akalianzisha tena, “Nchi ngumu hii, kwanza mmepuliza mipafyumu kila mtu na yake, harufu kali hazieleweki, madirisha mmefunga ili tufe mfurahi yaani hii Nchi watu kama wamerogwa.”
Kiliibuka kicheko cha wengi huku waliokuwa wamefunga kabisa madirisha kuhofia kuloana wakilegeza misimamo kwa kuyafungua kidogo, bila shaka maneno yaliwaingia kwani kuna jirani yangu alisemesha, “ujue Brother mambo mengine ni kutukia akili fupi tu, yani hutaki kuloana ili ukose hewa safi kweli?. wakati mwingine tujiongeze tu,” alisisitiza jirani.
Wakati huu mimi akili yangu haikuwa hapo Kabisa, nilikuwa nikimuwaza Bosi wangu Geofrey Mwaijonga jinsi ambavyo huwa anaamini katika akili ndogo, huwa nakubaliana naye 50 kwa 50 lakini baadaye nikajiuliza hivi kwanini watu wanaochukulia mambo kiurahisi hufanikiwa zaidi, kuliko wale wanaoyaangalia mambo kwa upana? nikagundua kumbe yupo sahihi.
Kumbe, hata kwenye Daladala akili ndogo ikitumika ugomvi na mabishano yasiyo na msingi vitapungua, katika utendaji kazi mkishirikiana na mkatumia akili ndogo mtafikia malengo, Dereva barabarani akili ndogo akiitumia hata ajali zitatoweka, Majumbani, Nyumba za Ibada, Shughuli za kijamii nk, akili ndogo ikitumika hakika mambo ni Super.