Kocha mkuu wa timu ya Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa malengo yao ni kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Mara ya mwisho Hall kuiongoza Azam FC kwenye michuano hiyo, ilikuwa ni mwaka juzi walipofika hatua ya 16 bora, kabla ya kutolewa na FAR Rabat ya Morocco kwa jumla ya mabao 2-1 ugenini.

Azam FC ingeweza kusonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano kama nahodha wake, John Bocco, angeifunga penalti iliyopata timu hiyo dakika za mwisho lakini akagongesha mwamba huku mabeki wake wawili, David Mwantika na Wazir Salum wakilimwa kadi nyekundu.

Hall ameiambia azamfc.co.tz kuwa anataka kuivusha Azam FC kwa kuipeleka mbele zaidi alipoishia mara ya mwisho kwenye michuano hiyo na anaamini kwa ubora wa kikosi alichokuwa nacho atafanikisha hilo.

“Kipindi cha mwisho nilipokuwa hapa tulifika hatua ya 16 bora, na kutolewa na timu kutoka Morocco, tulifaidi mengi kupitia safari hiyo, hata wachezaji nao walijifunza mengi, tulienda Sudan, Liberia na Morocco, ilitupa uzoefu mkubwa kama klabu kwa kuwa timu yetu ilikuwa bado changa.

“Hivyo malengo tuliyojiweka kwa mashindano yajayo, ni kufika hatua ya makundi, na naamini kikosi bora nilichokuwa nacho tunaweza kufikia malengo hayo,” alisema Hall.

Azam FC imeshindwa kufikia mafanikio hayo kwa miaka miwili mfululizo tokea Hall alipoondoka, mrithi wake Joseph Omog aliishia raundi ya kwanza na kusitishiwa mkataba wake Februari mwaka huu baada ya kutolewa na El Merreikh (Sudan) katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, mpaka sasa imefanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) ikiwa kileleni kwa jumla ya pointi 25 baada ya kushinda mechi nane na sare moja.

Picha: Muonekano Wa Lupita Nyong’o Gumzo Kwenye ‘Glamour Women Of The Year Awards’
Victoria Beckham aonesha mapenzi yake Beckham kwenye jukwaa la ‘Glamour Awards’