Kampuni ya kopafasta Microfinance Limited, imetoa ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Oktoba 12, 2022 kuhusu utapeli unaofanywa na baadhi ya watu na makampuni kupitia mitandao na tayari wamewasilisha barua rasmi BRELA kuwaomba kuufahamisha umma kuhusu uhalali wa kopafasta Microfinance Limited.
Akizungumza na vyombo vya Habari hii leo Oktoba 13, 2022 Meneja Mtendaji wa Kampuni ya kopafasta Microfinance Limited, Patrick Kang’ombe amesema jina lililotajwa na BRELA ambalo ni ‘Kopa Fasta Company Limited’, halina uhusiano wowote na kampuni hiyo.
Amesema, Kampuni yake ilisajiliwa kwa kuzingatia sheria kwa jina la ‘KOPAFASTA MICROFINANCE LIMITED’ na kupewa cheti cha usajili Namba 138564851 kilichotolewa na Msajili wa Makampuni – BRELA Agosti 9, 2019.
Kang’ombe amefafanua kuwa, Kopafasta Microfinance Limited inaisihi jamii kuepuka matapeli ambao wengi hutumia mitandao ya kijamii na kwamba wasikubali kulipa kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya kupata mkopo, mbinu ambayo ni maarufu na inayotumiwa na matapeli kujipatia fedha kwa kutumia majina batili yenye mfanano na majina halisi.
Amesema, “Mikopo inayotolewa na kampuni yetu hutumia vigezo vinavyozingatia sheria za nchi, hakuna anayepaswa kutoa fedha ili kupata mikopo hiyo na kupitia taarifa hii tunawasihi watanzania wanaohitaji kupata mikopo mbalimbali kupitia Kopafasta Microfinance Limited kupiga simu namba 0742 024 747.”
“Lakini pia unaweza kufika katika ofisi zetu zilizopo 373, barabara ya Garden, Mikocheni na tafadhali, toa taarifa haraka kwa vyombo vya usalama unapobaini jaribio la utapeli.”
Kupitia sehemu ya taarifa ya BRELA, iliyolenga kutoa ufafanuzi kuhusu kampuni ya Kalynda e-commerce Limited Oktoba 12, 2022, ilieleza kuwa, “hivi karibuni kumekuwa na tabia ya watu wasio waaminifu kughushi vyeti vya Makampuni, Majina ya Biashara na Leseni za Biashara kwa lengo ovu la kuwatapeli wananchi.”
Taarifa hiyo, ilifafanua kwamba, “Baadhi ya vyeti vilivyoghushiwa ni pamoja na Kopa Fasta Company Limited, Champion Investment na Afric. Taarifa zimeshatolewa kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya hatua za kijinai.”