Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya makubaliano kati ya Serikali na Kampuni tatu za madini kutoka Perth Nchini Australia ambapo amesema Tani milioni 18.5 zenye asilimia 4.5 ya madini adimu yamegundulika katika Kijiji cha Ngwala Songwe na yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 20.
Akiongea hii leo April 17, 2023 baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Ikulu Chamwino jijini Dodoma Rais Samia amesema yapo maeneo ambayo zamani yaliaminika ni masikini yasiyo na rutuba na yasiyo na vyanzo vingine vya fedha, kumbe mali ipo chini ya ardhi.
Amesema, “Mikoa ya Lindi na Morogoro ipo katika ukanda wa madini Kinywe (Graphite) na Mkoa wa Songwe upo katika ukanda wenye madini adimu “rare earth element” ndio maana miradi hii ipo Chilalo (Lindi), Epanko Wilayani Ulanga na Ngwala wilayani Songwe.”
Aidha Rais Samia ameongeza kuwa, “hadi sasa kuna kiasi cha mashapo cha tani milioni 67 zenye wastani wa asilimia 5.4 ya madini ya Kinywe, yaliyogunduliwa katika kijiji cha Chilalo kilichopo Lindi, ambayo yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 18.