Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania – TASAC, limetoa elimu kwa wananchi juu ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
Kaimu Afisa Mfawidhi, Mkoa wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Joseph Myaka ameyasema hayo wakati wa maonesho ya Bishara, Uwekezaji na Fursa yanayofanyika katika viwanja vya Mashujaa kuanzia Machi 19 – 31, 2023 Mkoani Mtwara.
Amesema, TASAC pia imeshiriki maonesho hayo ili kuwapa elimu wananchi kuhusu fursa za biashara zilizopo katika Sekta ya Usafiri kwa njia ya Maji, sambamba na elimu kuhusu Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa mazingira majini jukumu linalotekelezwa na Shirika hilo.
“TASAC tunashiriki maonesho haya ya Biashara Uwekezaji na Fursa mkoani Mtwara na kutoa elimu kwa wananchi kama mdhibiti wa shughuli za usafiri kwa njia ya maji tunasimamia huduma zinazotolewa na Bandari, tunadhibiti na kusimamia ulinzi, usalama na utunzaji wa mazingira na kuratibu shughuli za uokoaji na utafutaji pale panapotokea dhoruba majini,” amesema Mhandisi Joseph
Aidha ameongeza kuwa, “pia tunatoa elimu kwa wananchi wa Mtwara na wadau wa usafiri kwa njia ya maji katika jukumu letu la Udhibiti wa Safari kwa njia ya Maji na udhibiti Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira majini, wanaweza kufanya shughuli zao kwa usalama na kupata maendeleo na kuongeza pato la Taifa.”
Kwa mujibu wa Sheria, TASAC ina wajibu wa kusimamia kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhimiza usimizi na shughuli za uwakala wa meli wenye ufanisi, kuhimiza shughuli za bandari na huduma za meli zenye ufanisi, kuhakikisha kunakuwepo usalama na ulinzi wa shehena, kuhimiza na kutunza mazingira, usalama na ulinzi wa bahari, maziwa na mito.
Maonesho hayo ya uwekezaji na fursa ni ya kwanza kufanyika Mkoani humo yakiwa na lengo la kuwaleta pamoja wadau mbalimbali katika Sekta hiyo, ili kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kujifunza biashara na uwekezaji wa kisasa pamoja na fursa zilizopo katika sekta hiyo na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla.